Thesis and dissertation
Permanent URI for this collection
Browse
Recent Submissions
- ItemUchunguzi wa Sababu na Athari za Kutafautiana Kwa Idadi ya Fonimu na Viashiria Vyake Katika Kiswahili Sanifu(Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania, 2023) ABDALLA, Khamis AmourUtafiti huu ulichunguza sababu na athari za kutafautiana kwa idadi ya fonimu na viashiria vyake katika Kiswahili sanifu. Uchunguzi huu ulifanyika kutokana na kuwagundua wataalamu zaidi ya 35 waliotafautiana katika uwasilishaji wao wa idadi ya fonimu na viashiria vya Kiswahili sanifu. Malengo mahsusi ya utafiti huu ni kubaini sababu, athari na mapendekezo ya tatizo la kuofautiana kwa wataalamu katika uwasilishaji wa idadi ya fonimu na viashiria vya Kiswahili sanifu. Nadharia ya Lyons (1968) ya Umbo-Sauti Maumbo Kimatumizi pamoja na kanuni ya Trubetzkoy (1939/1969) ya Nitoe Nikutoe katika Jozi Sahili ziliongoza utafiti huu. Data zilikusanywa kutoka maktabani na nyanjani. Sampuli ilikuwa na Wasailiwa 115 walioteuliwa kutoka vyuo vikuu vya SUZA, ZU, SU na MNMA. Data zilichambuliwa kwa kutumia mbinu za maelezo, majedwali na magrafu. Utafti ulibaini sababu 14 na athari 15 za kutafautiana kwa idadi ya fonimu na viashiria vyake katika Kiswahili sanifu. Sababu kuu ni ile ya wataalamu kutoainisha kanuni inayowasilisha idadi ya fonimu na athari kuu ni ile ya kuibua mgogoro wa kuwachanganya na kuwababaisha wahadhiri, wanataaluma na wasomi wa vyuoni kwa kutojuwa idadi gani ni sahihi kati ya 27, 28, 29, 30, 31, 32, 33, 34, 35, 36, 37, 38, 40, 41, 42, 45 na 58. Utafiti pia uligundua kuwa kutafautiana kwa idadi ya fonimu na viashiria vyake, kumetokana na wataaalamu zaidi ya 35 kuwasilisha baadhi ya fonimu ambatano ambazo hazikubaliki kuwa ni fonimu baada ya kupimwa kwa kanuni ya kisayansi inayowasilisha idadi sahihi ya fonimu na viashiria vyake. Utafiti umethibitisha kwamba, kanuni ya Nitoe Nikutoe katika Jozi Sahili za maneno ni ya kisayansi na ni suluhisho la kuwasilisha idadi ya fonimu za Kiswahili sanifu. Kanuni hii itaweza kuziba pengo la kutafautiana kwa idadi ya fonimu na viashiria vyake katika Kiswahili sanifu. Utafiti ulipendekeza wataalamu wa fonolojia ya Kiswahili sanifu wakiongozwa na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, wakae pamoja na kukubaliana kuhusu idadi moja ya fonimu na viashiria vyake kulingana na nadharia na kanuni muwafaka. Mabaraza ya Kiswahili yamesisitizwa yasimamie kwa makini sera ya Kiswahili na kuupitia upya usanifishaji wa Kiswahili ili kuweka makubaliano ya pamoja na kuepukana na tatizo la kutafautiana kwa idadi ya fonimu na viashiria vyake katika Kiswahili sanifu.
- ItemKAULI ZA NASAHA KATIKA HARUSI ZINAVYOJENGA UHUSIANO WA WANANDOA:(SUZA, 2021-12-01) BIROLI,FATMA YAKOUTUtafiti huu ulikuwa na lengo la kuchunguza kauli za nasaha katika harusi za Wapemba jinsi zinavyojenga uhusiano wa wanandoa. Utafiti ulikuwa na malengo mawili: Kuainisha kauli za nasaha anazopewa biharusi na bwanaharusi kwa mujibu wa utamaduni wa jamii ya Wapemba na kufafanua uhusiano wa ndoa unaojengwa na kauli hizo. Utafiti uliongozwa na nadharia ya uchambuzi makini wa matini. Utafiti ulifanyika katika wilaya mbili, Chake chake na Mkoani. Data zilikusanywa kupitia mbinu ya dodoso, usaili na ushuhudiaji. Sampuli ya watafitiwa thelathini (30) ilitumika. Utafiti umebaini kuwa kauli za nasaha zitolewazo katika harusi za Wapemba. Ziko kauli za nasaha ambazo zimefanana na zinajenga uhusiano baina ya biharusi na bwanaharusi katika maisha ya ndoa. Mfano “Jihadhari sana, usimruhusu mke kuwa na marafiki wengi na kutumia muda mwingi nje kwa kukaa na marafiki zake.” “Tahadhari sana na ulimi, tunakunasihi, ulimi wako unatakiwa utumie vizuri.” Pia mtafiti amegundua kauli za nasaha zimefanikiwa kuonesha uhusiano unaojengwa na kauli hizo kwa bwanaharusi na biharusi. Mfano wa kauli za nasaha zinazojenga uhusiano kwa bwanaharusi na biharusi: “Tunakunasihi, mke ni mkeo, ndio mwenzio usimfanyie jeuri wala dharau.” “Zingatia vizuri tunayokunasihi, umuheshimu mumeo umuone ni mumeo wala simdharau.” Mtafiti anapendekeza kuwa kauli za nasaha ziendelee kutumika katika jamii ya Wapemba na jamii nyengine za Waswahili. Pia mtafiti anapendekeza uchunguzi zaidi ufanyike katika uwanja wa kitaaluma utakaohusisha kauli za nasaha katika miktadha tafauti ikiwemo msibani, maofisini, mashuleni na miktadha mengineo ili kuzijenga jamii kuwa na maadili bora katika sehemu zote napokuwepo. Pia mtafiti anapendekeza watafiti wengine waangalie kauli za nasaha walizopewa wanandoa wakongwe na wanandoa wa sasa halafu walinganishe wepi waliofanikiwa kudumu katika ndoa zao.
- ItemTATHMINI YA UTOAJI WA MAELEZO YA UTAMADUNI KATIKA KUFUNDISHA KISWAHILI KAMA LUGHA YA KIGENI(SUZA, 2019-12-01) ALI,Yakuti NassorUtafiti huu umeshughulikia; Tathmini ya Utoaji wa Maelezo ya Utamaduni katika Kufundisha Kiswahili kama Lugha ya Kigeni. Maelezo ya utamaduni ni kipengele muhimu sana katika ufundishaji wa lugha. Maelezo hayo yamebainishwa kwa ufupi katika vitabu kulingana na mada husika. Mwalimu amepewa nafasi ya kutoa maelezo ya ziada kuhusu utamaduni kwa kutumia mbinu alimbali. Utafiti umefanywa Unguja, Mkoa wa Mjini Magharibi katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Taasisi ya Kiswahili na Utamaduni (KIU). Lengo la utafiti huu lilikuwa ni kubainisha aelezo ya utamaduni yanayotolewa katika ufundishaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni, kutathmini mbinu anazotumia mwalimu kutoa maelezo ya utamaduni katika kufundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni na kueleza umuhimu wa maelezo ya utamaduni katika kufundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni. Jumla ya watoa taarifa tisa (9) walihusiswa kutoa taarifa katika utafiti huu. Watoa taarifa hao ni walimu wanaofundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni ambao walichaguliwa kwa kutumia sampuli lengwa kulingana na upatikanaji wao. Data zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya mahojiano, ushuhudiaji na uchambuzi ws nyaraka. Utafiti uliongozwa na nadharia ya utamaduni jamii iliyotumika kuangalia maelezo ya utamaduni kama kitu kipya na muhimu nachotakiwa kupewa mwanafunzi katika ufundishaji lugha na mbinu za utoaji wa maelezo ya utamaduni katika kufundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni. Utafiti ulitathmini na kushughulikia utoaji wa maelezo ya utamaduni kwa wanafunzi wa kiwango cha kwanza. Matokeo ya utafiti yamebaini kuwa: walimu wanatumia mbinu mbalimbali kutoa maelezo ya utamaduni lakini mbinu zinazotumika haziwasaidii sana walimu kufundisha wanafunzi wa kiwango cha kwanza kwa urahisi zaidi. Utafiti umependekeza walimu wapewe mafunzo ya kutosha kuhusu utoaji wa maelezo ya utamaduni na matumizi ya mbinu ya teknolojia katika utoaji wa maelezo ya utamaduni kama vile televisheni na mkazo zaidi utolewe kwa walimu wanaofundisha wanafunzi wa kiwango cha kwanza
- ItemTATHMINI YA MAZINGIRA YA KIJAMII KATIKA KUJIFUNZA KUSOMA KISWAHILI KWA WATOTO WA KIGENI ZANZIBAR(SUZA, 2019-12-01) ALI,Msellem MohammedUtafiti huu umetathmini Mazingira ya Kijamii katika kujifunza kusoma kwa watoto wa kigeni wanaojifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni Zanzibar. Jumla ya watoa taarifa 28 walishiriki katika utafiti huu waliogawanyika katika makundi mawili: wajifunzaji lugha 16 na wazazi/walezi wao 12. Utafiti ulifanyika katika skuli ya Kimataifa ya Feza iliyopo Mjini Magharib Zanzibar na katika kaya za wazazi/walezi wa wajifunzaji lugha ya Kiswahili zilizopo Mjini Magharib. Katika kukusanya data, utafiti umetumia kipimo cha kusoma ili kubaini uwezo walionao watoto wa kigeni katika kusoma matini za Kiswahili pamoja na mbinu ya usaili kubaini dhima ya Mazingira ya Kijamii. Aidha, utafiti ulitumia hojaji za kuchunguza mambo ya Mazingira ya Kijamii wa watoto wa kigeni. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Ukuzaji Stadi ya Kusoma ya Clay (1966) na Holdaway (1979). Hoja kuu ya nadharia hii ni mchangamano wa kimazungumzo na kusoma pamoja baina ya anayejifunza kusoma na wajuzi wa lugha husika. Vilevile, mchangamano baina ya mjifunzaji kusoma na vitabu vya lugha lengwa ni miongoni mwa misingi mikuu ya ujifunzaji kusoma kwa mujibu wa Nadharia ya Ukuzaji Stadi ya Kusoma. Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba dhima ya Mazingira ya Kijamii katika kujifunza kusoma Kiswahili kwa watoto wa kigeni ni kuwawezesha watoto kupata kuchanganyika na marafiki wanaojua Kiswahili wakiwa katika Mazingira ya Kijamii. Aidha, kuchanganyika na wazazi/walezi wanaotumia Kiswahili pamoja na tabia binafsi ya watoto kujisomea maandiko ya Kiswahili wakiwa katika Mazingira ya Kijamii pia vimechangia uwezo wa kusoma walionao watoto wa kigeni. Vilevile, imependekezwa kwa watafiti wengine kufanyika utafiti kuhusu ufundishaji na ujifunzaji wa stadi nyengine za lugha ya Kiswahili katika Mazingira ya nje na ndani ya darasa.
- ItemMKABALA UNAOTUMIKA KATIKA UTUNGAJI WA MITIHANI YA KISWAHILI KAMA LUGHA YA KIGENI:(SUZA, 2020-12-01) MGASHO,Makame ShehaUtafiti huu unahusu Mkabala Unaotumika Katika Utungaji wa Mitihani ya Kiswahili Kama Lugha ya Kigeni: Mfano Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar. Utafiti huu uliongozwa na malengo mahsusi matatu. Kwanza kufafanuakwa kiasi gani walimu wanaotunga maswali ya mitihani ya Kiswahili kwa wageni wanavyoifahamu mikabala ya utungaji mitihani. Pilikubainisha aina ya mkabala unaotumika zaidi katika utungaji wa maswali ya mitihani ya Kiswahili kw wageni. Tatu kuchunguza mtazamo wa walimu juu ya mkabala wanaoutumia zaidi katika utungaji wa maswali ya mitihani ya Kiswahili kwa wageni. Utafiti huu ulifanywa katika Idara ya Kiswahili kwa Wageni Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar. Nadharia iliyotumika katika utafiti huu ilikuwa Nadhari ya Tabia ya Umoja (Unitary Trait Hypothesis) kama ilivyoasisiwa na Oller (1979).Misingi mikuu ya nadharia hii ni kuipima lugha kwa njia ya mjumuishi pamoja na uzingatiaji wa mazingira halisi ya watumiaji wa lugha inayohusika wakati wa upimwaji wake.Sampuli ya utafiti huu ilikuwa ni walimu saba wanaosomesha Kiswahili kwa wageni, watoa taarifa hao walipatikana kwa usampulishaji tajwa. Mbinu zilizotumika ni mbinu ya dodoso kwa ajili ya kukusanya data za lengo la kwanza hadilengo la tatu, na mbinu ya uchambuzi wa nyaraka ilitumika kwa ajili ya kukusanya data za lengo la pili tu la utafiti huu. Matokeo ya utafiti huu yalieleza kwamba walimu wanaosomesha Kiswahili kwa wageni wanaufahamuwa mikabala ya utungaji mitihani ya Kiswahili kama lugha ya kigeni kwa asilimia 57%. Pia utafiti ulionesha kwamba mkabala unaopima stadi nyingi za lugha kwa wakati mmoja ndio ambao hutumika zaidi, na mtazamo wa walimu kuhusu mkabala unaotumika zaidikwamujibu wa matokeo ya utafiti ni wenye kufaa kwani unawapatia matokeo wanayoyahitaji katika upimaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni. Utafiti huu ulitoa mapendekezo ya kwamba walimu waongeze taaluma yao juu ya mikabala ya upimaji, pamoja na uzingatiaji wa stadi zotekuunne za lugha katika upimaji wa wanafunzi ili kuhakikisha kwamba hakuna stadi ya lugha hata moja ambayoinaachwa nyuma wakati wa upimaji wa wanafunzi.