Uchunguzi wa Sababu na Athari za Kutafautiana Kwa Idadi ya Fonimu na Viashiria Vyake Katika Kiswahili Sanifu
No Thumbnail Available
Date
2023
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania
Abstract
Utafiti huu ulichunguza sababu na athari za kutafautiana kwa idadi ya fonimu na viashiria vyake katika Kiswahili sanifu. Uchunguzi huu ulifanyika kutokana na kuwagundua wataalamu zaidi ya 35 waliotafautiana katika uwasilishaji wao wa idadi ya fonimu na viashiria vya Kiswahili sanifu. Malengo mahsusi ya utafiti huu ni kubaini sababu, athari na mapendekezo ya tatizo la kuofautiana kwa wataalamu katika uwasilishaji wa idadi ya fonimu na viashiria vya Kiswahili sanifu. Nadharia ya Lyons (1968) ya Umbo-Sauti Maumbo Kimatumizi pamoja na kanuni ya Trubetzkoy (1939/1969) ya Nitoe Nikutoe katika Jozi Sahili ziliongoza utafiti huu. Data zilikusanywa kutoka maktabani na nyanjani. Sampuli ilikuwa na Wasailiwa 115 walioteuliwa kutoka vyuo vikuu vya SUZA, ZU, SU na MNMA. Data zilichambuliwa kwa kutumia mbinu za maelezo, majedwali na magrafu. Utafti ulibaini sababu 14 na athari 15 za kutafautiana kwa idadi ya fonimu na viashiria vyake katika Kiswahili sanifu. Sababu kuu ni ile ya wataalamu kutoainisha kanuni inayowasilisha idadi ya fonimu na athari kuu ni ile ya kuibua mgogoro wa kuwachanganya na kuwababaisha wahadhiri, wanataaluma na wasomi wa vyuoni kwa kutojuwa idadi gani ni sahihi kati ya 27, 28, 29, 30, 31, 32, 33, 34, 35, 36, 37, 38, 40, 41, 42, 45 na 58. Utafiti pia uligundua kuwa kutafautiana kwa idadi ya fonimu na viashiria vyake, kumetokana na wataaalamu zaidi ya 35 kuwasilisha baadhi ya fonimu ambatano ambazo hazikubaliki kuwa ni fonimu baada ya kupimwa kwa kanuni ya kisayansi inayowasilisha idadi sahihi ya fonimu na viashiria vyake. Utafiti umethibitisha kwamba, kanuni ya Nitoe Nikutoe katika Jozi Sahili za maneno ni ya kisayansi na ni suluhisho la kuwasilisha idadi ya fonimu za Kiswahili sanifu. Kanuni hii itaweza kuziba pengo la kutafautiana kwa idadi ya fonimu na viashiria vyake katika Kiswahili sanifu. Utafiti ulipendekeza wataalamu wa fonolojia ya Kiswahili sanifu wakiongozwa na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, wakae pamoja na kukubaliana kuhusu idadi moja ya fonimu na viashiria vyake kulingana na nadharia na kanuni muwafaka. Mabaraza ya Kiswahili yamesisitizwa yasimamie kwa makini sera ya Kiswahili na kuupitia upya usanifishaji wa Kiswahili ili kuweka makubaliano ya pamoja na kuepukana na tatizo la kutafautiana kwa idadi ya fonimu na viashiria vyake katika Kiswahili sanifu.
Description
PhD YA KISWAHILI-LUGHAWIYA