Thesis and dissertation

Permanent URI for this collection

Browse

Recent Submissions

Now showing 1 - 5 of 5
  • Item
    Changamoto Zinazowakabili Walimu katika Ufundishaji wa Kiswahili kama Lugha ya Kigeni katika Stadi ya Kusoma
    (SUZA, 2019-12-01) Suleiman Khalfan, Shani
    Lengo kuu la utafiti huu ni kuchunguza changamoto zinazowakabili walimu katika ufundishaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni katika Stadi ya Kusoma. Utafiti huu umefanywa katika Idara ya Kiswahili kwa Wageni ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Kituo cha Kiswahili na Utamaduni (KIU) katika tawi lake la Zanzibar. Mtafiti alitumia nadharia ya stadi ya kusoma ya Schema iliyoasisiwa na Barlett (1932) na kuungwa mkono na Rumelhart na Ortony (1977). Washiriki wa utafiti huu walikuwa ni walimu wanaofundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni katika Chuo Kikuu cha Zanzibar, Idara ya Kiswahili kwa Wageni na Kituo cha Kiswahili na Utamaduni. Mbinu za ukusanyaji data alizotumia mtafiti katika utafiti huu ni dodoso, usaili na ushuhudiaji. Matokeo ya utafiti yamebaini kuwa walimu wanakabiliwa na changamoto nyingi katika ufundishaji wa stadi ya kusoma; kama ukosefu wa vifaa vya kufundishia, walimu kukosa mbinu za kisasa katika ufundishaji na ugumu wa matini zinazotumika kufundishia stadi ya kusoma. Changamoto hizo zimesababisha walimu kuumia muda mwingi katika ufundishaji, kutofikia malengo ya ufundishaji waliyojiwekea, kukosa ari, hamu na shauku ya kuendelea kufundisha na kutumia nguvu za ziada. Utafiti huu umetoa mapendekezo kuwa ili ufundishaji wa stadi ya kusoma uwe na ufanisi, taasisi husika zinapaswa kutoa mafunzo ya mara wa mara kwa walimu, uandaaaji wa vifaa vya kisasa vya ufundishaji vinavyokwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia ya ufundishaji lugha. Walimu wajijengee tabia ya kujisomea na kujifunza kupitia mitandao badala ya kusubiri nafasi za ufadhili.
  • Item
    Tathmini ya Utoaji wa Maelezo ya Utamaduni katika Kufundisha Kiswahili kama Lugha ya Kigeni
    (SUZA, 2019-12-01) Nassor Ali, Yakuti
    Utafiti huu umeshughulikia; Tathmini ya Utoaji wa Maelezo ya Utamaduni katika Kufundisha Kiswahili kama Lugha ya Kigeni. Maelezo ya utamaduni ni kipengele muhimu sana katika ufundishaji wa lugha. Maelezo hayo yamebainishwa kwa ufupi katika vitabu kulingana na mada husika. Mwalimu amepewa nafasi ya kutoa maelezo ya ziada kuhusu utamaduni kwa kutumia mbinu mbalimbali. Utafiti umefanywa Unguja, Mkoa wa Mjini Magharibi katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Taasisi ya Kiswahili na Utamaduni (KIU). Lengo la utafiti huu lilikuwa ni kubainisha maelezo ya utamaduni yanayotolewa katika ufundishaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni, kutathmini mbinu anazotumia mwalimu kutoa maelezo ya utamaduni katika kufundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni na kueleza umuhimu wa maelezo ya utamaduni katika kufundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni. Jumla ya watoa taarifa tisa (9) walihusiswa kutoa taarifa katika utafiti huu. Watoa taarifa hao ni walimu wanaofundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni ambao walichaguliwa kwa kutumia sampuli lengwa kulingana na upatikanaji wao. Data zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya mahojiano, ushuhudiaji na uchambuzi ws nyaraka. Utafiti uliongozwa na nadharia ya utamaduni jamii iliyotumika kuangalia maelezo ya utamaduni kama kitu kipya na muhimu anachotakiwa kupewa mwanafunzi katika ufundishaji lugha na mbinu za utoaji wa maelezo ya utamaduni katika kufundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni. Utafiti ulitathmini na kushughulikia utoaji wa maelezo ya utamaduni kwa wanafunzi wa kiwango cha kwanza. Matokeo ya utafiti yamebaini kuwa: walimu wanatumia mbinu mbalimbali kutoa maelezo ya utamaduni lakini mbinu zinazotumika haziwasaidii sana walimu kufundisha wanafunzi wa kiwango cha kwanza kwa urahisi zaidi. Utafiti umependekeza walimu wapewe mafunzo ya kutosha kuhusu utoaji wa maelezo ya utamaduni na matumizi ya mbinu ya teknolojia katika utoaji wa maelezo ya utamaduni kama vile televisheni na mkazo zaidi utolewe kwa walimu wanaofundisha wanafunzi wa kiwango cha kwanza.
  • Item
    Changamoto za Ufundishaji na Ujifunzaji wa Kiswahili kama Lugha ya Kigeni katika Darasa Mseto la Wingilugha
    (SUZA, 2019-12-01) Hamad Saleh, Fatma
    Utafiti huu ulichunguza changamoto za ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni katika darasa mseto la wingilugha. Ulibainisha changamoto za walimu katika ufundishaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni katika darasa mseto la wingilugha, changamoto za wanafunzi katika kujifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni katika darasa mseto la wingilugha na kufafanua namna walimu wanavyokabiliana na changamoto katika kufundisha na wanafunzi katika kujifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni katika darasa mseto la wingilugha. Utafiti huu ulitumia nadharia ya viwezeshi katika masomo ya wingilugha. Utafiti huu ulifanyika Zanzibar, katika kisiwa cha Unguja. Data zilikusanywa katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar katika Idara ya Kiswahili kwa Wageni. Watoa taarifa wa utafiti huu ni walimu waliotoka katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, katika Idara ya Kiswahili kwa Wageni na wanafunzi wanaojifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni chuoni hapo. Data za msingi zilikusanywa kwa njia ya usaili na ushuhudiaji na katika uchambuzi wake ulitumika mkabala wa kimaelezo. Matokeo ya utafiti huu yalibaini kuwa walimu wanapata changamoto katika kufundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni katika darasa mseto la wingilugha. Miongoni mwao ni walimu kukosa ujuzi wa kutosha wa ufundishaji wa darasa kama hili, ugumu wa kutafsiri wanapokuwa wanafundisha na kulazimika kuchanganya lugha, tafauti za kitamaduni, na nyinginezo. Utafiti ulibaini kuwa wanafunzi wanapata changamoto za tafauti za kiutamaduni, hadhi zao, athari ya lugha ya kwanza katika kujifunza lugha ya Kiswahili. Utafiti ulipendekeza kuwa; walimu wapatiwe mafunzo ya kutosha katika kufundisha Kiswahili kwa wanafunzi wanaojifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni hasa darasa mseto la wingilugha, walimu wajifunze lugha nyengine za kigeni pamoja na utamaduni wake. Vilevile wawe na ubunifu wa kutumia mbinu na viwezeshi muafaka pamoja na zana za kisasa kwa madarasa kama haya. Kwa upande wa wanafunzi kuzungumza lugha ya Kiswahili darasani, kuheshimu utamaduni wa kila mwanafunzi, kutotilia maanani tafauti ya mwanafunzi mmoja na mwengine na nyenginezo.
  • Item
    Mikakati binafsi ya Kujifunza Lugha Inayomsaidia Mwanafunzi wa Kigenu Kuzungumza Lugha ya Kiswahili
    (SUZA, 2019-12-01) Mustafa Fatawi, Zakia
    IKISIRI Utafiti huu ulilenga kuchunguza mikakati binafsi ya kujifunza lugha inayomsaidia mwanafunzi wa kigeni kuzungumza lugha ya Kiswahili. Utafiti ulifanyika Zanzibar katika kisiwa cha Unguja katika Mkoa wa Kusini Unguja na Mkoa wa Mjini Magharibi. Utafiti huu una malengo mahususi matatu ambayo ni kuelezea mitazamo ya wanafunzi wanaojifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni wakati wanapojiwekea mikakati yao binafsi ya kujifunza kuzungumza lugha ya Kiswahili. Kutathmini ni kwa kiasi gani wanafunzi wanaojifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni wanatumia mikakati binafsi katika kujifunza kuzungumza Kiswahili. Kubainisha mikakati binafsi ambayo ni sahihi inayotumiwa na wanafunzi wanaojifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni ambayo inawawezesha kuweza kuzungumza lugha ya Kiswahili. Jumla ya walengwa wa utafiti huu ni watafitiwa (15) ambao ni wastani wa (75%). Watafitiwa hawa walipatikanwa katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Taasisi ya Mafunzo ya Kiswahili ya Paje na wageni ambao tayari wameshajifunza Kiswahili wamepatikana maeneo ya Mji Mkongwe kwa kutumia uteuzi wa usampulishaji rahisishi. Hojaji na Usaili zilitumika kama mbinu za kukusanyia data za utafiti huu. Mtafiti alitumia nadharia ya Utamaduni Jamii na nadharia Tete Ingizo. Data zilipatikanwa uwandani na zilifafanuliwa kwa kutumia mkabala wa mseto. Matokeo ya utafiti huu yalionesha kuwa (93.3%) ya wanafunzi wanaojifunza kuzungumza lugha ya Kiswahili wanatumia mikakati binafsi na mikakati hiyo ni sahihi lakini hawana uelewa wa kutosha wa utumiaji wa mikakati ya kujifunza lugha. Asilimia kubwa ya watafitiwa hutumia mkakati jamii katika kujifunza kwao. Mtafiti amependekeza kwa watafiti wengine kuchunguza mikakati binafsi ya kujifunza lugha ambayo humsaidia mwanafunzi wa kigeni kusikiliza, kusoma na kuandika. Pia watafiti wachunguze mikakati binafsi wanayoitumia walimu katika kuwafundisha wanafunzi wa kigeni lugha ya Kiswahili. Pendekezo jingine ni kwa Uongozi wa chuo ama taasisi waweke program endelevu ya rafiki lugha ili mwanafunzi aweze kuzungumza kwa haraka zaidi na kuujuwa utamaduni wa lugha ya Kiswahili.
  • Item
    Tathmini ya Ziada za Kimasoma katika Ufundishaji wa Kiswahili kama Lugha ya Kigeni: Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar
    (SUZA, 2019-12-01) ALI, SALIM A.
    Utafiti huu unahusu tathmini ya ziara za kimasomo katika ufundishaji wa Kiswahilili kama lugha ya kigeni; Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar. Ziara zilizochunguzwa ni ziara za kimasomo zinazoendeshwa katika Idara ya Kiswahili kwa Wageni ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar. Utafiti ulifanywa katika wilaya ya mjini Unguja, Zanzibar katika Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar. Data zilipatikana kwa njia ya usaili na ushuhudiaji. Watoa taarifa walikuwa ni walimu wanaofundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni SUZA pamoja na wanafunzi wa kigeni wanaojifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni chuoni hapo. Mbinu zilizotumika zilisaidia kupata data za kutosha ambazo baadae zilichambuliwa kwa njia ya maelezo na kukamilisha malengo ya utafiti. Malengo hayo ni kubainisha hatua za kitaaluma zinazofuatwa katika kuwaandaa wanafunzi kwenda katika ziara za kimasomo katika ufundishaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni, kuchambua mambo wanayofanya wanafunzi wakati wa ziara za kimasomo katika ufundishaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni na kutathmini ni kwa namna gani ziara za kimasomo zinawasaidia wanafunzi katika kujifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni. Mtafiti alisoma kazi tangulizi mbalimbali na zilimsaidia kupata mwanga wa kufanya kazi yake kwa kujua mambo mbalimbali yaliyoandikwa awali kuhusiana na ziara za kimasomo. Nadharia jamii katika kujifunza ilitumika kukusanya na kuchambua data zilizopatikana katika kazi hii. Utafiti umedhihirisha kuwa kuna hatua kadhaa zinazofuatwa katika kuwaandaa wanafunzi kwenda katika ziara za kimasomo katika ufundishaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni ambazo zinasaidia idara kudhibiti vyema ziara hizo. Hatua hizo ni kutoa ratiba ya siku ya ziara, kutoa mwongozo wa ziara na kuwapa wanafunzi maswali yanayohusu ziara watakayokwenda.