Thesis and dissertation
Permanent URI for this collection
Browse
Browsing Thesis and dissertation by Subject "2. Mbinu za ufundishaji kiswahili kwa wageni"
Now showing 1 - 2 of 2
Results Per Page
Sort Options
- ItemTathmini ya Mbinu za Kufundishia Stadi ya Kuandika Kiswahili kama Lugha ya Kigeni Zanzibar:(The State University of Zanzibar (SUZA), 2019-12) KAHINDI, Saada SaidUtafiti huu ulifanyika kisiwani Unguja, katika Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, taasisi mbili zilichanguliwa kushiriki katika utafiti huu. Moja ya taasisi hiyo ni ya kiserikali na nyengine ni taasisi binafsi. Lengo kuu la utafiti huu ni kutathmini mbinu wanazozitumia walimu katika kufundisha stadi ya kuandika Kiswahili kama lugha ya kigeni kwa kuzingatia kipengele cha utungaji. Watafitiwa katika utafiti huu walikuwa ni walimu wanaofundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Taasisi ya Kiswahili na Kiswahili na Utamaduni (KIU) ambazo kieneo zote zinapatikana Zanzibar. Mbinu mbalimbali za kukusanyia data ambazo ni usaili, dodoso na ushuhudiaji zilitumika katika kupata data zenye uhakika na zenye kuaminika. Matokeo ya utafiti yamebainisha kuwa, ni kweli kuna mbinu ambazo walimu wanazitumia katika kufundishia stadi ya kuandika. Walimu wanatumia mbinu kama vile mbinu ya picha, hadithi, ziara za kimasomo, barua na mbinu jumuishi/mseto katika kufundisha stadi ya kuandika Kiswahili kama lugha ya kigeni hasa katika kipengele cha utungaji. Kutokana na matokeo na mapendekezo ya utafiti pamoja na watafitiwa imegundulika kwamba walimu hawana mafunzo ya kutosha juu ya stadi za lugha, pia muamko katika ufundishaji wa stadi ya kuandika ni mdogo sana ingawa mbinu za kufundishia zipo wazi bado kunahitajika ushajihishaji wa hali ya juu kwa wanafunzi. Katika utafiti huu, mtafiti alipendekeza taasisi zenye dhima ya kufundisha Kiswahilikama lugha ya kigeni Zanzibar, zijaribu kuandaa warsha za mafunzo ya mbinu za kufundishia stadi za lugha hasa stadi ya kuandika.Hali hii itasaidia walimu katika kuboresha ufundishaji wao wa stadi hii na stadi nyengine za lugha. Mwisho kabisa, mtafiti alishauri tafiti nyengine zifanyike ili kuziba pengo lililoachwa na watafiti wengine, na watafiti wajikite zaidi katika stadi za lugha hasa Kiswahili kama lugha ya kigeni.
- ItemUgumu wa Kufundisha Stadi ya Kusikiliza kwa Wanafunzi wa Kigeni Wanaojifunza Kiswahili:(The State University of Zanzibar (SUZA), 2019-11) NASSOR, Fatma SoudUtafiti huu unahusu Ugumu wa kufundisha Stadi ya Kusikiliza kwa Wanafunzi Wageni Wanaojifunza Kiswahili: Mfano Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). Utafiti ulikuwa na lengo la kuangalia mambo makuu matatu. Kwanza, kubaini mbinu wanazotumia walimu wakati wa kufundisha stadi ya kusikiliza. Pili, kupambanua ugumu unaowakabili walimu wa Idara ya Kiswahili kwa Wageni katika kufundisha stadi ya kusikiliza. Tatu kupendekeza mikakati itakayoweza kusaidia kuimarisha stadi ya kusikiliza. Utafiti ulifanyika Idara ya Kiswahili kwa Wageni (SUZA). Utafiti uliongozwa na “Modeli ya Ufundishaji Lugha Kimaakazi” kama ilivyoasisiwa na Echevarria, Vogt na Short, 2000; 2013).Utafiti ulitumia mbinu ya ushuhudiaji, mahojiano na uchambuzi wa nyaraka katika kupata data. Sampuli ya watoa taarifa walikuwa ni walimu wanaofundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni katika kiwango cha kati. Matokeo yanaonesha kuwa walimu hutumia mbinu zifuatazo: Kusikiliza redio na kisha kujibu maswali, kusikiliza nyimbo na baadaye kujibu maswali, kufanya imla, kutumia simu kusikiliza habari na kisha kujibu maswali, kualika mgeni, ziara za kimasomo, kumsikiliza mwalimu kusoma matini na baadaye kufanya mazoezi ya oral (kutamka) kufundisha stadi ya kusikiliza. Kadhalika, matokeo ya utafiti huu yanaonesha kwamba upo ugumu unaowakabili walimu katika kufundisha stadi ya kusikiliza. Ugumu huo ni pamoja na kuchukua muda katika matayarisho, ukosefu wa maabara ya lugha na vifaa vingine vya ufundishaji, mtaala kutoelekeza ufundishaji wa stadi ya kusikiliza, kukosekana kwa mafunzo ya jinsi ya kufundisha stadi ya kusikiliza kwa walimu, mazingira ya darasa, utayari wa wanafunzi na tofauti ya kiwango cha uelewa wa wanafunzi. Aidha, ili kuimarisha ufundishaji wa stadi ya kusikiliza imependekezwa mikakati ifuatayo: Mabadiliko ya mtaala na vitabu vya kufundishia, mafunzo kwa walimu yatolewe mara kwa mara, utumiaji wa teknolojia na vifaa vya kisasa, kupewa hadhi sawa stadi zote za lugha na kufanya tathmini katika stadi ya kusikiliza. Mapendekezo yaliyotolewa ni pamoja na utumiaji wa ufarafuzi wa vifaa, kufanya utafiti katika stadi nyingine za lugha kama vile kusoma, kuzungumza na kuandika, kuangalia ugumu wa stadi ya kusikiliza katika viwango vingine. Mapendekezo hayo yatachangia kwa kiasi kikubwa ufundishaji wa Kiswahili ikiwa lugha ya kigeni utafundishwa vizuri kwa kuzingatia stadi zote za lugha bila ya kuibagua hata moja hususan stadi ya kusikiliza.