TATHMINI YA MIKAKATI YA MARAFIKI WA LUGHA KWA WANAFUNZI WA KISWAHILI KAMA LUGHA YA KIGENI ZANZIBAR

No Thumbnail Available
Date
2020-11-01
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
SUZA
Abstract
Wanafunzi wengi wanaokuja kujifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni wana nafasi chache za kushirikiana na wazawa ambao ni wazungumzaji wa lugha mama ya Kiswahili. Mara nyingi uelewa kwenye lugha unapatikana kwa kutumia mbinu mbali mbali za ufundishaji wa lugha ya pili au ya kigeni ambayo humpa mwanafunzi wa kigeni kupata stadi za kusoma, kusikiliza, kuzungumza na kuandika. Mbinu hizi huweza kuwasaidia wanafunzi hawa kujifunza lugha kwa ufasaha kutoka kwa wazawa. Mbinu moja wapo ni kutumia mkakati wa marafiki wa lugha kwa wanafunzi wanaojifunza kama Kiswahili kama lugha ya kigeni. Njia hii huweza kuwasaidia wanafunzi hawa kujifunza lugha kwa ufasaha kutoka kwa wazawa. Kwa mantiki hiyo lengo kuu la utafiti huu ni kutathmini kwa kiasi gani mikakati inayotumiwa na marafiki wa lugha huwasaidia wanafunzi wa kigeni kujifunza Kiswahili kwa ufasaha katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). Utafiti ulikuwa na malengo matatu mahsusi. Kwanza, kubainisha majukumu ya marafiki wa lugha yaliyoandaliwa na Idara ya Kiswahili kwa Wageni; pili, kuchunguza mikakati inayotumiwa na marafiki wa lugha katika kuwasaidia wanafunzi wa kigeni kujifunza Kiswahili katika Chuo cha SUZA1.Tatu, kutathmini viwango vya usaidizi walivyovipata wanafunzi wa kigeni kutoka kwa marafiki wa lugha ya Kiswahili. Utafiti uliongozwa na nadharia ya Mwingiliano Jamii iliyoasisiwa na Vygostsky miaka ya 1980. Utafiti huu ulifanyika Kisiwa cha Unguja, Mkoa wa Mjini Magharibi kwa kuhusisha watoa taarifa wazawa. Vilevile, ulishirikisha wanafunzi wa kigeni wanaoishi nchi ya Marekani waliowahi kushiriki katika programu ya marafiki wa lugha katika chuo hiki uanzia 2010 mpaka 2018. Utafiti ulihusisha makundi matatu na watoa taarifa 28. Aliyekuwa mkuu wa Idara ya Kiswahili kwa Wageni, marafiki wa lugha ya Kiswahili 15 na wanafunzi wa kigeni waliowahi kushiriki programu ya marafiki wa lugha ya Kiswahili kutoka nchi ya Marekani walikuwa 12. Data za utafiti zilikusanywa kwa mbinu ya usaili na hojaji. Matokeo ya utafiti huu yameeleza kwamba mbinu ya kutumia marafiki wa lugha katika kujifunza na kufundisha Kiswahili kwa wanafunzi wa kigeni hurahisisha mchakato wa kufundisha na kujifunza. Wanafunzi wa kigeni huzifahamu vyema stadi za Kiswahili. Marafiki wa lugha waliandaa mikakati mahsusi katika kuwasaidia wanafunzi wa kigeni kujifunza Kiswahili kwa wepesi. Baadhi ya mikakati hiyo ni mkakati wa kiziara, mkakati wa kushiriki matukio ya kijamii, mkakati wa usomaji matini za Kiswahili, mkakati wa usikilizaji na utazamaji wa filamu za Kiswahili. Kutokana na matokeo ya utafiti huu mtafiti alipendekeza kuwa mbinu ya marafiki wa lugha, ni vyema kutumika kwa wanafunzi wote wa Kiswahili kama lugha ya kigeni. Aidha kwa sasa mbinu hiyo hutumiwa kwa wanafunzi wachache wanaokuwa tayari kuichagua na kuilipia mbinu hiyo katika masomo yao. Hivyo, utafiti huu unapendekeza mbinu hii itumike kwa wanafunzi wote wa kigeni katika kujifunza Kiswahili hapa SUZA. Vilevile, mbinu hii iimarishwe kwa kuongezwa muda wa kukutana baina ya marafiki wa lugha na wanafunzi wa kigeni ili ipatikane fursa kubwa ya kujifunza Kiswahili. Aidha, utafiti unapendekeza kutolewa kwa mafunzo zaidi ambayo ni endelevu kwa marafiki wa lugha ili kupunguza changamoto na hatimaye kuleta ufanisi wa hali ya juu katika programu hiyo.
Description
Wanafunzi wengi wanaokuja kujifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni wana nafasi chache za kushirikiana na wazawa ambao ni wazungumzaji wa lugha mama ya Kiswahili.
Keywords
Citation