TATHMINI YA MIKAKATI YA MARAFIKI WA LUGHA KWA WANAFUNZI WA KISWAHILI KAMA LUGHA YA KIGENI ZANZIBAR
Loading...
Date
2020-11-01
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
SUZA
Abstract
Wanafunzi wengi wanaokuja kujifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni wana nafasi chache za
kushirikiana na wazawa ambao ni wazungumzaji wa lugha mama ya Kiswahili. Mara nyingi
uelewa kwenye lugha unapatikana kwa kutumia mbinu mbali mbali za ufundishaji wa lugha
ya pili au ya kigeni ambayo humpa mwanafunzi wa kigeni kupata stadi za kusoma, kusikiliza,
kuzungumza na kuandika. Mbinu hizi huweza kuwasaidia wanafunzi hawa kujifunza lugha
kwa ufasaha kutoka kwa wazawa. Mbinu moja wapo ni kutumia mkakati wa marafiki wa
lugha kwa wanafunzi wanaojifunza kama Kiswahili kama lugha ya kigeni. Njia hii huweza
kuwasaidia wanafunzi hawa kujifunza lugha kwa ufasaha kutoka kwa wazawa. Kwa mantiki
hiyo lengo kuu la utafiti huu ni kutathmini kwa kiasi gani mikakati inayotumiwa na marafiki
wa lugha huwasaidia wanafunzi wa kigeni kujifunza Kiswahili kwa ufasaha katika Chuo
Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). Utafiti ulikuwa na malengo matatu mahsusi. Kwanza,
kubainisha majukumu ya marafiki wa lugha yaliyoandaliwa na Idara ya Kiswahili kwa
Wageni; pili, kuchunguza mikakati inayotumiwa na marafiki wa lugha katika kuwasaidia
wanafunzi wa kigeni kujifunza Kiswahili katika Chuo cha SUZA1.Tatu, kutathmini viwango
vya usaidizi walivyovipata wanafunzi wa kigeni kutoka kwa marafiki wa lugha ya Kiswahili.
Utafiti uliongozwa na nadharia ya Mwingiliano Jamii iliyoasisiwa na Vygostsky miaka ya
1980. Utafiti huu ulifanyika Kisiwa cha Unguja, Mkoa wa Mjini Magharibi kwa kuhusisha
watoa taarifa wazawa. Vilevile, ulishirikisha wanafunzi wa kigeni wanaoishi nchi ya
Marekani waliowahi kushiriki katika programu ya marafiki wa lugha katika chuo hiki uanzia
2010 mpaka 2018. Utafiti ulihusisha makundi matatu na watoa taarifa 28. Aliyekuwa mkuu
wa Idara ya Kiswahili kwa Wageni, marafiki wa lugha ya Kiswahili 15 na wanafunzi wa
kigeni waliowahi kushiriki programu ya marafiki wa lugha ya Kiswahili kutoka nchi ya
Marekani walikuwa 12. Data za utafiti zilikusanywa kwa mbinu ya usaili na hojaji. Matokeo
ya utafiti huu yameeleza kwamba mbinu ya kutumia marafiki wa lugha katika kujifunza na
kufundisha Kiswahili kwa wanafunzi wa kigeni hurahisisha mchakato wa kufundisha na
kujifunza. Wanafunzi wa kigeni huzifahamu vyema stadi za Kiswahili. Marafiki wa lugha
waliandaa mikakati mahsusi katika kuwasaidia wanafunzi wa kigeni kujifunza Kiswahili kwa
wepesi. Baadhi ya mikakati hiyo ni mkakati wa kiziara, mkakati wa kushiriki matukio ya
kijamii, mkakati wa usomaji matini za Kiswahili, mkakati wa usikilizaji na utazamaji wa
filamu za Kiswahili. Kutokana na matokeo ya utafiti huu mtafiti alipendekeza kuwa mbinu ya
marafiki wa lugha, ni vyema kutumika kwa wanafunzi wote wa Kiswahili kama lugha ya
kigeni. Aidha kwa sasa mbinu hiyo hutumiwa kwa wanafunzi wachache wanaokuwa tayari
kuichagua na kuilipia mbinu hiyo katika masomo yao. Hivyo, utafiti huu unapendekeza mbinu
hii itumike kwa wanafunzi wote wa kigeni katika kujifunza Kiswahili hapa SUZA. Vilevile,
mbinu hii iimarishwe kwa kuongezwa muda wa kukutana baina ya marafiki wa lugha na
wanafunzi wa kigeni ili ipatikane fursa kubwa ya kujifunza Kiswahili. Aidha, utafiti
unapendekeza kutolewa kwa mafunzo zaidi ambayo ni endelevu kwa marafiki wa lugha ili
kupunguza changamoto na hatimaye kuleta ufanisi wa hali ya juu katika programu hiyo.
Description
Wanafunzi wengi wanaokuja kujifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni wana nafasi chache za
kushirikiana na wazawa ambao ni wazungumzaji wa lugha mama ya Kiswahili.