Kiwango cha ukubalifu wa Istilahi za Kiswahili za Technolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar :

No Thumbnail Available
Date
2017-11
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
The State University of Zanzibar (SUZA)
Abstract
Utafiti huu unahusu “Kiwango cha ukubalifu wa istilahi za kiswahili za Teknolojia ya habari na mawasiliano, Zanzibar: mfano kutoka istilahi za Kilinux”. Utafiti huu umejikita katika kuchunguza mambo matatu ambayo: Mosi, kuelezea ukubalifu wa istilahi za TEHAMA zilizoundwa chini ya mradi wa Kilinux miongoni mwa Wazanzibari. Pili kufafanua matumizi halisi ya istilahi za Kiswahili za TEHAMA kwa watumiaji walioko katika sekta ya elimu Zanzibari. Tatu kubainisha endapo kuna istilahi nyingine za TEHAMA zinazotumika zisizo za Kilinux. Utafiti huu umeongozwa na Nadharia ya Istilahi za Kisayansi (NIK) iliyoasisiwa na K.B. Kiingi (1989). Nadharia hii ina sifa maalum ambazo zinasisitiza usasa wa istilahi za lugha, Pia imeweza kujaliza Nadharia ya Istilahi ya Jumla (NIJ) ya Wuester (1931). Ambayo imeeleza kwamba katika uundaji wa istilahi ni lazima muundaji azingatie vigezo fulani vya istilahi zinazofaa, hivyo basi ni Nadharia inayowaongoza wanaistilahi kuunda, kukubali na kukataa istilahi fulani za Kiswahili, hasa zile zisizokuwa na usayansi yaani zile zisizoelezeka kimantiki kwa mujibu wa vigezo tisa vya kisayansi ambavyo hujulikana kama PEGITOSCA ambapo kwa Kiswahili vimefupisha na kuitwa SIZAMASTALIHA yaani usahihi, uiktisadi, uzalishi, umataifa, uangavu, ustaara, utaratibu, ulinganifu na uhalisia. Utafiti huu umefanyika katika taasisi za elimu ya juu zilizoko Zanzibar, vikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha SUMAIT na Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) . Matokeo ya Utafiti yanaonesha kwamba katika maeneo matatu ya kitaaluma yaliyofanyiwa utafiti kiwango cha ukubalifu wa istilahi za TEHAMA za Kiswahili ni kidogo. Sababu kuu ni ugumu na kutoeleweka kimantiki kwa istilahi hizo. Vilevile baadhi ya mbinu za uundaji istilahi zilizotumika zimepelekea kuundwa istilahi ambazo sio rahisi kueleweka. Vilevile mazoea yalioko kwa watumiaji wa TEHAMA ya kutumia lugha chanzi (Kiingereza) pia ni miongoni mwa sababu ya kutokutumika kwa istilahi hizo za Kiswahihili. Aidha kasumba juu ya lugha ya Kiswahili nazo pia ni kikwazo.Kwa mujibu wa utafiti huu istilahi ambazo zimeonekana kukubalika ni zile zilizotafsiriwa au kutoholewa. Pia kuna istilahi ambazo zimezoeleka kutumika zinazotofautiana na zile zilioundwa na mradi (Kilinux). Kwa matokeo haya imebainika kwamba katika jamiilugha ya waswahili walioko Zanzibar hususani wanataaluma, ambao ni watumiaji wakubwa TEHAMA, ni wachache ambao wanakubaliana na istilahi za TEHAMA za Kiswahili zilizoundwa na mradi wa Kilinux. Taarifa hii imeenda sambamba na tathmini nyingine kama vile (Alloni-Feinberg, 1974; Ohly,1979; Mdee, 1980; Mwansoko, 1990; 1993; Sewangi, 1996; Were-Mwaro,2001) zimedhihirisha kuwa baadhi ya Istilahi zilizoundwa rasmi huweza kukataliwa au kutokukubalika na watumiaji wa lugha husika. Licha ya juhudi kubwa ambazo wataalamu wamefanya katika kuisaidia jamii kutumia maarifa haya mapya (TEHAMA) kwa kutumia lugha yao ya Kiswahili, juhudi hizo kwa upande wa Zanzibar zimeonekana kutofanikiwa kama ilivyokusudiwa. Kwa hivyo zoezi la uundaji istilahi lihusishe wanaistilahi na watumiaji wake. Hoja hii imekaziwa nguvu na Mwansoko (1990) kwa kusema, wenye kuhitaji istilahi (watumiaji wa lugha) hawasubiri kuundiwa istilahi na vyombo vya ukuzaji istilahi bali hujiundia istilahi zao wenyewe pale haja inapozuka. Kutokana na hayo, waundaji istilahi wanapaswa kufanya utafiti zaidi juu ya baadhi ya istilahi nyingine ambazo hazijafanyiwa utafiti, ili waweze kuwasaidia watumiaji wa mtandao kwa lugha ya Kiswahili kwa kuunda istilahi rahisi ambazo zitakuwa ni rahisi kueleweka, kukubalika na kutumika vizuri.
Description
Available in print form, Tunguu Reference Library
Keywords
1. Istilahi za Kiswahili 2. Istiahi za sayansi ya Kompyuta na TEHAMA
Citation
Ulfat Abdulaziz Ibrahim